Friday, May 10, 2013

UFAFANUZI KUHUSU KUPITIWA UPYA KWA MATOKEO YA MTIHANI WA KIDATO CHA NNE MWAKA 2012

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

UFAFANUZI KUHUSU KUPITIWA UPYA KWA MATOKEO YA MTIHANI WA KIDATO CHA NNE MWAKA 2012

Mnamo tarehe 03 Mei, 2013 Serikali kupitia Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Mheshimiwa Wiliam Lukuvi (Mb) ilitoa Kauli ya Serikali Bungeni Kuhusu Taarifa ya Awali ya Tume ya Taifa ya Kuchunguza Sababu za kushuka kwa ufaulu wa Mtihani wa Kidato cha Nne Mwaka 2012. Kauli ya Serikali ilielekeza kuwa matokeo ya Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne mwaka 2012 yafutwe na yaandaliwe upya kwa kutumia utaratibu uliotumika mwaka 2011 ili Wanafunzi hao wawe katika mazingira yanayofanana na ya wenzao wa miaka iliyopita kwa kuwa mfumo uliotumika mwaka 2012 katika kupanga matokeo na madaraja ni tofauti na ule uliotumika mwaka 2011 na miaka iliyotangulia.