Monday, June 11, 2012

WAZIRI SAITOTI NA NAIBU WAKE WAFARIKI DUNIA

Profesa George Saitoti enzi za uhai wake

Waziri wa Usalama wa ndani Profesa George Saitoti na Naibu wake Orwa Ojode wamefariki dunia katika ajali ya helikopta ya polisi iliyotokea leo asubuhi katika eneo la Kibiku, karibu na mji wa Ngong takriban kilometa ishirini kutoka mji mkuu wa Nairobi. Abiria wote sita, wakiwemo marubani wawili na walinzi wa mawaziri hao waliokuwa kwenye helikopta hiyo wamefariki dunia na miili yao kuteketezwa kwa kiasi cha kutoweza kutambulika. Kilichosababisha ajali hiyo bado hakijabainika.
Bwana Saitoti na maafisa wengine wa juu katika wizara ya usalama wa ndani walikuwa wakielekea katika eneo la Sotik kwa mkutano wa usalama. Saitoti alikuwa miongoni mwa wanasiasa mashuhuri nchini Kenya waliokuwa wakipania kugombea kiti cha urais katika uchaguzi mkuu ujao.
Walioshuhudia ajali hiyo wamesema waliona helikota hiyo ikizunguka angani kabla ya kuanguka katika msitu wa Ngong. Polisi wamezingira eneo la ajali hiyo na kamishna wa polisi Mathew Iteere aliyepo katika eneo la ajali anatarajiwa kutoa taarifa kamili kuhusiana na ajali hiyo.
Ajali hiyo ya helikopta imetokea katika siku ambapo Kenya inaadhimisha miaka minne tangu kutokea ajali ya ndege iliyowauwa mawaziri wengine wa serikali, Kipkalya Kones na Lorna Laboso.