Friday, October 21, 2011

MWISHO WA GADDAFI


ALIYEKUWA kiongozi wa Libya, Kanali Muammar Gaddafi ameripotiwa kuuawa na wapiganaji wanaoongozwa na Baraza la Mpito nchini humo (NTC), baada ya mji wa nyumbani kwake, Sirte kunyakuliwa na vikosi hivyo jana.Kifo cha Kanali Gaddafi (69) kilitangazwa rasmi na Waziri Mkuu wa Serikali ya mpito nchini humo, Mahmoud Jibril, muda mfupi baada kiongozi huyo aliyeitawala Libya kwa miaka 42 kuuawa. Awali, msemaji wa NTC nchini Libya, Kanali Ahmed Bani alisema Kanali Gaddafi aliuawa na mwili wake ulipelekwa katika mji wa Misratah, bila kutoa ufafanuzi kamili kuhusu mazingira ya kifo hicho.Taarifa za kuuawa kwake zilitolewa huku zikiambatanishwa na picha zinazoonyesha sura inayoonekana kuwa ni ya kiongozi huyo, katika muonekano wa nywele zake laini na ndefu wastani na uso uliotapakaa damu na majeraha.Kanali Gaddafi anakuwa kiongozi wa kwanza kuuawa tangu kuanza vuguvugu la mageuzi katika mataifa ya kiarabu mwanzoni mwa mwaka huu, yaliyowaondoa madarakani Rais Ben Ali wa Tunisia na Hosni Mubarak wa Misri.Kifo hicho kimetangazwa ikiwa ni miezi tisa tangu kuanza kwa upinzani mkali dhidi ya Serikali yake Februari mwaka huu, ambapo aliapa kwamba asingeondoka nchini Libya na kwamba yeye na wafuasi wake wangepambana hadi tone la mwisho la damu.Kanali Gaddafi ambaye wakati wa utawala wake aliwahi kujipa wadhifa wa “mfalme wa wafalme wa Afrika” alikuwa akisifika kwa ukali wa sauti yake na maneno makali ya kuhamasisha na kueleza misimamo yake katika hotuba zake. Mapambano hayo yameishia katika mji wa nyumbani kwake, Sirte ambao umekuwa na upinzani mkali kwa vikosi vya wapiganaji wa NTC ambavyo vililazimika kupambana kwa miezi kadhaa hadi waasi walipofanikiwa kuuteka jana. Kanali Bani alisema mtoto wa Kanali Gaddafi, Mutassim ambaye walikuwa pamoja katika mji wa Sirte aliuawa na wapiganaji hao wa NTC. Msemaji huyo aliwaambia waandishi wa habari kuwa kiongozi huyo alifariki dunia baada ya kujeruhiwa vibaya katika miguu yake yote na kichwani. “Aliuawa katika mapambano na wapiganaji wetu. Kuna picha zinazoonyesha hayo,”alisema.Alijificha kwenye karavatiKwa mujibu wa taarifa za vyombo mbalimbali vya habari vya kimataifa, Kanali Gaddafi alidhibitiwa baada ya kukutwa  amejificha katika karavati la barabarani, yeye pamoja na baadhi ya walinzi wake.Kwa upande wake, kamanda wa wapiganaji wa baraza hilo, Abdul Hakim Belhaj pia alithibitisha kuwa Kanali Gaddafi alifariki dunia kutokana na majeraha aliyoyapata baada ya kukamatwa.Makamu Mwenyekiti wa NTC, Abdul Hafiz Ghoga alithibitisha mbele ya waandishi wa habari kuwa Gaddafi aliuawa katika mji wa Sirte.“Tunatangaza kwa dunia kuwa Muammar Gaddafi aliuawa katika mikono ya wanamapinduzi,” alisema Ghoga.Katika mtiririko wa matukio yaliyokuwa yakirushwa katika vituo mbalimbali vya televisheni, kituo cha televisheni cha al-Jazeera kilionyesha picha za mwili wa Kanali Gaddafi ukiburuzwa katika eneo alilouawa.Filamu za video zilizochukuliwa kwa simu za mkono zilionyesha kile kilichoonekana kuwa maiti ya Gaddafi iliyolowa damu. Mwili wake baadaye uliburuzwa na wapiganaji na kupakiwa nyuma ya gari aina ya pick-up. Nato na Marekani zilieleza kuwa haziwezi kuthibitisha taarifa za kuuwawa kwa kiongozi huyo ambaye hajaonekana tangu NTC ilipoikamata Tripoli.Watu washangilia mitaaniWakati huohuo, katika mji wa  Benghazi na miji mingine nchini humo, watu walionekana kukusanyika mitaani na kushangilia taarifa hizo za kuuawa kwa Gaddafi.Viongozi mbalimbali duniani pia wamezungumzia kuhusu taarifa hizo za kuuawa kwa Kanali Gaddafi ambaye amewahi kuwa mpinzani mkubwa wa mataifa ya Ulaya na Marekani kutokana na misimamo yake dhidi ya mataifa hayo.Miongoni mwa viongozi hao ni Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameroon ambaye alisema ni siku maalum ya kukumbuka maovu yote yaliyofanywa na Gaddafi.Alisema watu wa Libya wako katika nafasi nzuri ya kujenga nchi imara na yenye demokrasia.“Ninafurahi kazi ambayo Uingereza imesaidia katika kuuondoa utawala wa Gaddafi,”alisema.Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Alain Juppe amepongeza kufikiwa mwisho kwa utawala wa miaka 42 ya Gaddafi.Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon pia alisema kwamba kifo cha Kanali Gaddafi kinatoa mwanya wa “historia mpya kwa Libya”.“Watu wanatakiwa watambue kuwa huu ni mwisho wa mwanzo. Sasa ni wakati wa Walibya wote kushikamana na kuwa kitu kimoja. Ni wakati wa kuponya majeraha na kujenga upya taifa. Si wakati wa visasi,” alisema Ki-Moon.Balozi wa Libya nchini Uingereza, Mahmud Nacua alisema kuwa kuawa kwa Gaddafi kunamaanisha Libya inaelekea kwenye mustakhabali bora wa baadaye.Wasifu wa Kanali Muammar Gaddafi. Alikuwa mtoto wa wafugaji wa Kibedui, mwenye maisha ya utata, lakini ambaye alitukuzwa sana, huku mataifa ya Magharibi yakimuona mtu wa hatari wakati wote.Muammar Muhammad Gaddafi aliitawala Libya kwa zaidi ya miaka 40. Hadi mwanzoni mwa Machi 2011, alikuwa akiamini ndani ya moyo wake kwamba watu wake walikuwa wakimpenda na kwamba walikuwa tayari kumlinda hadi kufa kwa ajili yake. Lakini wakati huo, tayari Gaddafi alikuwa ameshatumia njia za kikatili kuyazima maandamano dhidi yake, maandamano ambayo baadaye yaligeuka vita vya wenyewe kwa wenyewe. Kwa mujibu wa taarifa, watu zaidi ya 30,000 waliuawa kwenye vita hivyo. Mara nyingi sana, Gaddafi alitoa matamko makali wakati wa vita hivyo, ila linalojuilikana zaidi ni lile la kuwaita wapinzani wake kuwa ni panya. Kwa kila hali, yaliyotokea ni mambo ambayo Gaddafi hakuyatarajia asilani. Mtoto huyu wa wafugaji wa Kibedui aliyezaliwa mwaka 1942, alikuja kuibuka kama mkombozi wa Walibya, alipompindua Mfalme Idriss hapo mwaka 1969. Kuanzia hapo akaanza kujenga kile alichokiona mwenyewe kuwa ni mfumo wa kidemokrasia wa moja kwa moja. Alianzisha kamati za umma zilizoamua juu ya mustakabali wa umma na wa Serikali. Aliuita mfumo wake wa kisiasa na kiuchumi kuwa ni wa kisoshalisti, alioufafanua kwenye kijitabu chake cha Kijani.