Wednesday, April 25, 2012

CHELSEA YAITOA BARCELONA UEFA


KATIKA kile kinachoonekana kumalizika kwa utawala wa Barcelona, mabingwa hao wa tetezi wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, wametolewa katika michuano hiyo baada ya kulazimishwa sare ya mabao 2-2 na Chelsea kwenye Uwanja wa Camp Nou, jana.
Kutokana na matokeo hayo Barcelona imevuliwa ubingwa rasmi na hivyo Chelsea imefanikiwa kutinga fainali ya michuano hiyo kwa jumla ya ushindi wa mabao 3-2, kutokana na ushindi wa Chelsea wa bao 1-0 kwenye Uwanja wa Stamford Bridge.
Chelsea ilicheza muda mwingi ikiwa pungufu baada ya nahodha wake, John Terry kutolewa kwa kadi nyekundu katika dakika ya 37 kutokana kumgonga Alexies Sanchez.
Chelsea ambayo ilitumia muda mwingi ikilinda lango lake ilipata mabao yake kupitia kwa Ramires na Fernando Torres, wakati  Barcelona ilipata mabao yake kupitia Sergio Busquets na Andres Iniesta.
Kipindi cha pili Barca ilipata penalti katika dakika ya 49, lakini Lionel Messi, aligongesha mwamba na mpira kuokolewa.
Torres aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Didier Drogba, ndiye aliyehitimisha safari ya Barca kutokana na bao lake katika dakika ya 90.
Kutokana na matokeo hayo, Chelsea inasubiri mshindi wa mchezo ya leo kati ya Real Madrid dhidi ya Bayern Munich.

No comments:

Post a Comment