Waziri
wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa (MB) leo ametangaza
rasmi matokeo ya Mitihani ya Kidato cha Nne, maarifa - QT.
TAARIFA YA MATOKEO YA MITIHANI YA MAARIFA (QT) NA KIDATO CHA NNE (CSEE)
ILIYOFANYIKA OKTOBA 2012
1.0 UTANGULIZI
Mitihani ya Kidato cha Nne (CSEE) na Maarifa (QT) kwa mwaka 2012 ilifanyika nchini kote kuanzia tarehe 8-25 Oktoba 2012. Napenda kuchukua nafasi hii kutangaza rasmi matokeo ya mitihani hiyo kama ifuatavyo :
2.0 MTIHANI WA MAARIFA (QT)
2.1 Usajili na Mahudhurio
Katika Mtihani wa Maarifa 2012 watahiniwa waliosajiliwa ni 21,310 ambapo wasichana walikuwa ni 13,134 na wavulana ni 8,176.
Jumla ya watahiniwa 17,137 sawa na asilimia 80.42 ya waliosajiliwa wamefanya Mtihani.
2.2 Matokeo ya Mtihani wa Maarifa (QT)
Watahiniwa 5,984 kati ya 17,137 waliofanya mtihani wamefaulu Mtihani wa Maarifa (QT).
3.0 MTIHANI WA KIDATO CHA NNE (CSEE) 2012
Jumla ya vituo 5,058 vilitumika katika kufanya Mtihani wa Kidato cha Nne 2012 ambapo vituo 4,155 vilikuwa vya watahiniwa wa shule na vituo 903 vilikuwa ni vya watahiniwa wa kujitegemea.
3.1 Usajili na Mahudhurio ya Watahiniwa
(a) Watahiniwa Wote
Jumla ya watahiniwa 480,036 walisajiliwa kufanya Mtihani wa Kidato cha Nne 2012 wakiwemo wasichana 217,583 sawa na asilimia 45.33 na wavulana 262,453 sawa na asilimia 54.67. Watahiniwa waliofanya mtihani wa Kidato cha Nne 2012 ni 456,137 sawa na asilimia 95.44. Watahiniwa 21,820 sawa na asilimia 4.55 ya watahiniwa wote waliosajiliwa hawakufanya mtihani.
(b) Watahiniwa wa Shule
Watahiniwa wa shule waliosajiliwa ni 411,230 wakiwemo wasichana 182,978 sawa na asilimia 44.50 na wavulana 228,252 sawa na asilimia 55.50. Watahiniwa wa shule waliofanya mtihani walikuwa 397,136 sawa na asilimia 96.57. Aidha, watahiniwa 14,090 sawa na asilimia 3.43 hawakufanya mtihani kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo utoro, ugonjwa na vifo.
(c) Watahiniwa wa Kujitegemea
Watahiniwa wa kujitegemea waliosajiliwa walikuwa ni 68,806 wakiwemo wasichana 34,605 sawa na asilimia 50.29 na wavulana 34,201 sawa na asilimia 49.71. Watahiniwa 61,001 wakiwemo wasichana 30,917 na wavulana 30,084 wamefanya mtihani wakati watahiniwa 7,730 sawa na asilimia 11.23 hawakufanya mtihani.
4.0 MATOKEO YA MTIHANI WA KIDATO CHA NNE
(a) Watahiniwa wa Shule
Jumla ya watahiniwa wa shule 126,847 kati ya watahiniwa 397,136 waliofanya Mtihani wa Kidato cha Nne 2012 wamefaulu. Wasichana waliofaulu ni 46,161 na wavulana ni 80,686.
(b) Watahiniwa wa Kujitegemea
Idadi ya watahiniwa wa kujitegemea waliofaulu mtihani ni 16,112 kati ya watahiniwa 61,001 waliofanya mtihani. Wasichana waliofaulu ni 6,751 na wavulana ni 9,361.
5.0 UBORA WA UFAULU KWA MADARAJA NA JINSI
Ubora wa ufaulu kwa kuangalia madaraja waliyopata watahiniwa wa shule unaonesha kuwa jumla ya watahiniwa 23,520 wamefaulu katika madaraja I – III ambapo kati yao wasichana ni 7,178 na wavulana ni 16,342.
Mchanganuo wa ufaulu kwa kila Daraja kwa jinsi kwa Watahiniwa wa Shule mwaka 2012 ni kama ifuatavyo: