Watu wa Usalama wakikagua ndani ya klabu hiyo.
Damu ikiwa imetapakaa katika klabu hiyo
WATU wapatao 14 wamejeruhiwa katika shambulio la guruneti lililotokea jana majira ya saa 7 usiku katika klabu ya Mwaura iliyopo mjini Nairobi, nchini Kenya. Imeripotiwa kuwa guruneti hilo lilirushwa na mtu asiyejulikana. Mtu huyo alifika kwenye eneo hilo la burudani na mlango ulipofunguliwa alirusha guruneti na kutokomea. "Jamaa mmoja aligonga mlango akijifanya kama mteja na aliporuhusiwa kuingia ndani, akarusha guruneti" alisema mkuu wa polisi mjini Nairobi, Bw. Anthony Kibuchi. Wengi wa majeruhi wa tukio hilo walikuwa na majeraha katika sehemu za mikono na miguu na walikimbizwa katika hospitali kuu ya taifa ya Kenyatta. Shambulio hili linatokea wiki moja baada ya vikosi vya Kenya kuingia nchini Somalia kukabiliana na wapiganaji wa al-Shabaab, ambao Kenya inawashutumu kwa mashambulio na utekaji nyara wa watalii. Al-Shabaab walitishia kufanya mashambulio kutokana na hatua hiyo ya Kenya.
No comments:
Post a Comment